Monday, December 5, 2011

Jaji Samatta Kutunuku Wahitimu 2220 Mzumbe University; Gazeti la Habari Leo


MKUU wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mkuu mstaafu Barnabas Samatta jana alitarajiwa kuwatunuku wahitimu 2,220 wa shahada mbalimbali.

Miongoni mwa wahitimu hao kwenye mahafali ya 10 ya chuo hicho mjini Morogoro wamo saba wa Shahada za Uzamivu (PhD).

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chuo hicho, Rainfrida Ngatunga alisema miongoni mwa wahitimu saba wa Shahada ya Uzamivu ni Waziri wa Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni, Dk. Emmanuel Nchimbi.

Wengine ni Gustav Kunkuta, Simon Lushakuzi, Sunday Makama kutoka Nigeria, George Makoma, Anarabbi Nangawe na Fred Rwechengula.

“Sisi kama chuo (Mzumbe) tunajivunia sana kuona namna uwiano wa jinsia kwa wahitimu unavyoshabihiana kwani kati ya wahitimu wote 1,282 wanaume na 938 wanawake,” alisema Ngatunga na kuongeza kuwa mahafali hayo yalitanguliwa na warsha chuoni hapo juzi.

Miongoni mwa mambo yaliyotarajiwa kufanywa juzi kwenye warsha ni kutambua michango mbalimbali ya wanazuoni waliofanya vizuri kwenye masomo na utafiti.

“Chuo chetu kitachukua fursa hiyo pia kutambua mchango wa Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa
(NHIF) katika ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike kwenye Kampasi Kuu Morogoro,” aliongeza.

Ngatunga alisema chuo pia kinatambua mchango mkubwa na uungaji mkono wa Benki ya CRDB katika mchakato mzima wa kuandaa kongamano la wadau wa elimu la chuo hicho lililofanyika Mei mwaka huu.

Akifafanua zaidi kuhusu mahafali hayo, Ngatunga alisema miongoni mwa wahitimu hao 1,365
watatunukiwa Kampasi Kuu Morogoro, wakati 47 watatunukia Shahada za Uzamili kwenye Shule ya Biashara ya Mzumbe iliyopo Dar es Salaam Desemba 16, na 383 watatunukiwa shahada zao kwenye Kampasi ya Mzumbe Mbeya Desemba 10, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment